Saturday, 8 September 2018

WADUDU WAHARIBIFU WA NYANYA NA DAWA ZAKE

Ili uweze kubaini mapema uwepo wa wadudu waharibifu au magonjwa katika mimiea yako ya nyanya ni lazima uwe unachunguza mimea yako mara kwa mara. Angalia uwepo wa wadudu kwenye sehemu ya chini ya majani, juu yake, kwenye mashina, maua au matunda kama yametobolewa au la.

Sasa ungana nami katika makala hii uweze kujua ni wadudu wepi waharibifu kwenye zao lako la nyanya shambani kwako ili uweze kukabiliana nao. Pia waweza kujua magonjwa ya nyanya na dawa zake hapa

1. Funza wa vitumba: American bollworm (Helicoverpa armigera)
Kubaini mapema mayai au funza kabla hayajatoboa matunda ni muhimu sana. Funza wachanga kwanza hula majani baadae matunda. Funza wakishaingia ndani ya matunda husababisha uharibifu mkubwa. Uharibifu kwenye matunda machanga husababisha kupukutika kwake, wakati mashambulizi ya matunda yaliyokomaa husababisha matundu ambayo huruhusu kuingia kwa aina nyingine za ukungu na bakteria ambao huleta madhara zaidi.





funza-wa-vitumba-anavyotoboa-matunda-ya-nyanya

Kipepeo chake huwa na rangi ya manjano-kahawia chenye doti iliyokoza, mistari isiyo sawa ya kijivujivu na alama nyeusi yenye umbile la figo kwenye mbawa za mbele. Mbawa za nyuma ni nyeupe na baka jeusi katika sehemu za nje. Kipepeo huwa na urefu wa 14-18mm na upana wa mbawa wa 35-40mm.

Namna ya kudhibiti
Kubainika mapema hupatikana kwa kuchunguza mazao kila mara. Angalia majani yaliyo chini ya maua ya juu yaliyochanua kwa kutafuta mayai ya viwavi tumba/dukari. Baada ya kubainika kwa funza huyu fuata mbinu zifuatazo:

Mbinu bora za kilimo
•Chuma na teketeza matunda yaliyoathirika.
•Ondoa na teketeza mabaki ya mazao baada ya kuvuna.
•Chimbulia ardhi baada ya mavuno.
•Fanya mzunguko wa mazao.
•Toa kwa mkono na teketeza mayai na funza wadogo wadogo.
•Epuka kupanda nyanya karibu na pamba au mahindi.
•Changanya mazao, panda na pilipili na maua bange (African marigold).

Dawa (Chemical control)
Mara nyingi dawa (kemikali) inayodumu kwa muda mfupi ndio inayohitajika kwani matunda hushambuliwa muda mfupi kabla ya kuvuna. Kwa hivyo, dawa kama vile mevinphos na endosulfan zinashauriwa kutumika. Dawa nyingine zilizosajiliwa kutumika kwa mdudu huyu ni carbaryl, tetrachlorvinphos, methomyl, acephate, monocrotophos na dawa zenye pareto.

Kibaiolojia (Biological control)
Funza wa vitumba wana maadui wengi asilia wakiwemo viumbe wanaokula mayai (kamaTrichogramma spp.), wanaoshambulia funza (nyigu na nzi wanaokula funza) na washambulizi kama vile aina za maji moto, assassin bugs, minute pirate (anthocorid) bugs, lacewings na ladybird beetles. Kuku na ndege pia hula mafunza na mabuu wakati fulani katika ukuaji wa matunda. Madawa ya kibaiolojia hujumuisha Muarobaini (Azadirachta indica) na Bt (Bacillus thuringiensis). Madawa yatokanayo na Bt yanayouzwa kwa udhibiti wa mafunza hujumuisha Dipel, Thuricide (zote ni aina za Bt kurstaki), Florbac 70 DG na XenTari (zote ni aina za Btaizawai).

2. Utitiri Mwekundu: Red spider mites  (Tetranychus urticae)
Utitiri wekundu huwa ni tatizo hasa wakati wa kiangazi. Utitiri huu unaweza kutambulika kwa kutumia lenzi ya mkono. Dalili za awali hujumuisha madoa ya manjano, ambayo hujitokeza pale mashambulizi yanapokuwa makubwa; baada ya hapo njano kubwa na ishara za kama kuungua hujitokeza kwenye majani na matunda ikifuatiwa na utando kama wa buibui.


Mashambulizi makubwa husababisha umanjano wa majani na matunda, kupukutika mapema kwa majani, kukauka kwa mti kuanzia kileleni na kufa kwa mmea. Vichungu vya utitiri wekundu hujikusanya kwenye ncha za majani wakati idadi ya utitiri wekundu inapozidi chakula kilichopo.

Namna ya kudhibiti
Fanya uangalifu wa kubaini utitiri wekundu kwenye mazao na chukua hatua mara unapowabaini. Matumizi ya dawa muafaka haraka pale tu utitiri wekundu wanapobainika, husaidia kupunguza athari.

Mbinu bora za kilimo
•Weka matandazo na mwagilia
•Ngo’a na choma moto mimea iliyoathirika
•Choma moto mabaki yote ya mazao baada ya kuvuna
•Fanya mchanganyiko wa mazao na vitunguu maji au vitunguu swaumu

Dawa (Chemical control)
Tumia dawa za kemikali pale tu utakapowabaini, na baada ya hapo tumia dawa za aina mbali mbali kwa kupishana kuzuia usugu wa utitiri wekundu. Aina nyingi za madawa zinaweza kutumika, kama vile Dimethoate, Abamectin, Bifenthrin na acephate.

Kibaiolojia (Biological control)
Aina ya utitiri shambulizi ni adui asilia wa utitiri wekundu anayepatikana kwenye maduka yanayouza viumbe washambulizi kwa matumizi kwenye jengo la kuoteshea mimea na hufanya kazi vizuri wanapodhibitiwa vyema. Hii inahitaji udhibiti mzuri bila ya kutumia madawa ya kemikali ya kuulia wadudu. Matumizi ya dawa za kemikali za kuulia wadudu zinaweza zikasababisha kutofanya kazi vizuri kwa viumbe hawa kwani wadudu wanaokula chawa wekundu huuliwa na dawa hizi.

3. Minyoo Fundo: Root knot nematodes (Meloidogynespp.)
Dalili za minyoo fundo hujumuisha kupiga umanjano na kudumaa kwa mimea na hatimaye kunyauka wakati wa jua kali. Mimea iliyoathirika hujitokeza shambani kwa sehemu sehemu. Mashambulizi husababisha kupungua kwa mazao ikitegemea ukubwa wa mashambulizi kwenye mizizi, mashambulizi makubwa husababisha kufa kwa mimea. Mimea huwa na stahimili ndogo kwa magonjwa mengine.



Mimea inapong’olewa kutoka kwenye udongo, mizizi huonekana imevimba yenye maumbile mabaya na vifundo, yanayojulikana kama mafundo ya mizizi. Ukubwa wa vifundo hivi unaweza kuwa sawa na ukubwa wa kichwa cha pini ya kirungu mpaka 25mm au zaidi. Mashambulizi makubwa husababisha mzizi wote ukawa na umbile baya na mafundo ambao hatimaye huoza. Mashambulizi yanayofuata husababisha uharibifu na dalili za magonjwa huongezeka kwenye nyanya.

Namna ya kudhibiti
Mimea mingi inayopandwa huwa na minyoo fundo. Minyoo huweza kuingizwa shambani kupitia miche kutoka vitaluni au kwa usambaaji kutoka shamba hadi shamba katika maeneo yenye mashambulizi. Hatua zifuatazo zinaweza kuchukuliwa ili kudhibiti minyoo ya mimea.

Mbinu bora za kilimo
•Tumia mimea ya mitego kama vile Mbange ‘marigold’ (Tagetes spp.) na haradali ya India.
•Dumisha kiwango kikubwa cha mbolea za asili (samadi na mboji) katika udongo.
•Changanya mashudu (mabaki) ya muarobaini na udongo.
•Tumia aina zenye kustahimili minyoo fundo (kama Caracas, Kentom, Meru, Piersol, Roma VFN, Tengeru 97, Zest F1, Star 9001 na Star 9003).
•Zungusha mazao na vitunguu maji, mahindi madogo, mahindi matamu, mahindi, mtama, uwele, ufuta, au nyasi. Mbinu ya mzunguko wa mazao unaojulikana kama “STRong” unashauriwa kutumika katika udhibiti wa minyoo fundo. Mbinu hii inashauri kupandwa kwa mmea usiostahimili (kama Nyanya), ikifuatiwa na zao lenye kustahimili kidogo (kama Kebeji), halafu zao lenye kustahimili kabisa (kama Vitunguu maji), kabla ya kurejea tena zao lisilostahimili (kama Nyanya).
•Ng’oa mizizi na uchome moto mimea iliyoathirika na takataka zote za mazao.
•Ua vimelea vya maradhi kwenye vitalu kwa kutumia moto au mvuke kabla ya kusia mbegu.
•Epuka kupandikiza miche iliyoathirika.
•Tumia mbinu za kibaiolojia kwa kutumia bidhaa zinazotokana na Trichoderma.

Dawa (Chemical control)
Minyoo fundo inaweza kudhibitiwa kwa kutumia dawa ya minyoo/wadudu (Vydate L) na dawa za kufukiza (Telone II, Telone C-17, Vapam), lakini hizi hazipatikani kwa urahisi.

Kibaiolojia (Biological control)
Udhibiti wa kibaiolojia unahusisha matumizi ya viumbe wapinzani wa minyoo fundo (kama ukungu na bacteria). Kuna aina nyingi za ukungu zinazokula minyoo. Baadhi ya aina za ukungu (Arthrobotryts spp. na Monacrosporium spp.) hutumia nyuzi zao na mbegu zinazoganda kama mitego ya kunasia minyoo, aina nyingine za ukungu (kama Pochonia chlamydosporia,Trichoderma spp. na Paecilomyces lilacinus) hufyonza mayai na minyoo jike. Aina za bakteria maarufu wapinzani wa minyoo ni Pasteuria penetrans na Bacillus spp.

4. Sota (Cutworms)
Hushambulia miche ya nyanya hasa baada ya kupandikizwa shambani. Wakati wa mchana hujificha kwenye udongo na usiku hujitokeza na kukata miche kwenye shina usawa wa udongo.


Namna ya kudhibiti
· Nyunyiza dawa za kuua wadudu (kama Rogor, Actellic, Selecron, Dursban) kwenye shina usawa wa udongo
· Hakikisha miche inapata maji ya kutosha

5. Vidukari au Wadudu mafuta (Aphids)
Ni wadudu wenye rangi nyeusi au kuijani au kahawia. Hukaa chini ya majani na kufyonza utomvu kwenye majani machanga. Hudumaza mmea na kushindwa kuzaa matunda
 
Namna ya kudhibiti
Nyunyizia dawa za sumu za kuulia wadudu kama Rogor, Actellic, Selecron, Dursban maji ya majani ya mwarobaini na utupa, maji ya pilipili.

6. Inzi weupe (White flies)
Hawa ni Inzi weupe wadogo sana. Hujitokeza sana wakati wa kiangazi. Wadudu hawa huenezaugonjwa wa nyanya wa virusi ujulikanao kama Rasta.

 Whiteflies-kwenye-jani-la-nyanya
Namna ya kudhibiti
Nyunyizia dawa za sumu za kuulia wadudu kama Selecron, Actellic, Dursban na thionex. Pia maji ya majani ya mwarobaini na utupa.

KILIMO BORA CHA KARANGA

Karanga ni zao muhimu la mafuta ambalo hutumika kama chakula cha binadamu. Mashudu na majani yake hutumika  kulisha mifugo. Pia hurutubisha udongo. Tanzania ni nchi ya pili kwa uzalishaji wa karanga Afrika baada ya nchi ya Nigeria. Karanga hustawi zaidi Mikoa ya Mtwara, Dodoma, Shinyanga na Tabora.


Mazingira ya ustawishaji
Karanga hustawi vizuri katika maeneo yenye mwinuko chini ya Mita 1500 kutoka usawa wa Bahari. Huhitaji mvua ya wastani wa milimita 500 – 1200 kwa mwaka. Pia hustawi vizuri kwenye udongo wa kichanga wenye rutuba.

Utayarishaji wa Shamba
Tifua vizuri shamba ili kuwezesha udongo kupenyesha maji na mizizi kirahisi. Karanga hupandwa kwenye matuta au sesa.

Kuchagua mbegu za kupanda
Hakikisha unapata mbegu bora za karanga zilizothibitishwa kitaalamu na kuainishwa na Taasisi za Utafiti wa Kilimo.

AINA ZA KARANGA
Kuna aina tisa za mbegu za karanga ambazo zimefanyiwa utafiti na kuidhinishwa zitumike kwa wakulima nazo ni:

Pendo 1998
Hukomaa kwa wastani wa siku 90 – 100 na hutoa mavuno ya wastani wa tani 1.5 kwa hekta. Ina mafuta ya wastani wa asilimia 48.

Naliendele 2009
Hukomaa kwa siku 90 – 100 na hutoa mavuno ya wastani wa tani 1 kwa hekta. Huvumilia ukame na ugonjwa wa ukoma.

Mangaka 2009
Hukomaa kwa siku 90 – 100. Huzaa mbegu 2 – 3 kwenye ganda moja. Hutoa mavuno wastani wa tani 1.5 kwa hekta. Ina mafuta wastani wa asilimia 48.

Mnanje 2009.
Hukomaa kwa siku 110 – 120. Hutoa mavuno ya wastani wa tani 1.5 kwa hekta. Ina mafuta wastani wa asilimia 51

Masasi 2009
Hukomaa kwa siku 110 – 120. Hutoa mavuno ya wastani wa tani 1 kwa hekta. Huvumilia ugonjwa wa ukoma na ina mafuta wastani wa asilimia 50.

Nachingwea 2009
Hukomaa kwa siku 110 – 120. Hutoa mavuno wastani wa tani 1 kwa hekta.

Nachi 2015
Hukomaa kwa siku 110. Hutoa mavuno wastani wa tani 1.1 – 2 kwa hekta. Huvumilia ugonjwa ya Ukoma

Kuchele 2013
Hukomaa kwa siku 102 – 110. Hutoa mavuno wastani wa tani 1.2 – 2 kwa hekta.  Huvumilia magonjwa ya Ukoma, kutu na madoa ya majani.

Narinut 2015
Hukomaa kwa siku 106 – 110. Hutoa mavuno wastani wa tani 1.2 – 2 kwa hekta. Huvumilia magonjwa ya Ukoma, kutu na madoa ya majani.

Upandaji
Mbegu zipandwe mapema wakati wa mvua za kwanza. Karanga zipandwe kwa nafasi ya entimita 10 kati ya mmea na sentimita 50 kati ya mstari. Kilo 80 hadi 100 za mbegu zitahitajika kupanda hekta moja kwenye shimo la kina kati ya sentimita 2.5 hadi 5.

Palizi
Palizi ya kwanza ifanyike majuma mawili baada ya karanga kuota. Palizi ifanyike mara mbili hadi tatu kuzuia magugu.

KUDHIBITI WADUDU NA MAGONJWA

Magonjwa
1.      Ugonjwa wa ukoma ( Rossette Virus diseases)
Huenezwa na wadudu waitwao Vidukari (aphids). Mimea inayoshambuliwa hudumaa, majani kukunjamana na kuwa na rangi ya manjano. Pia hupunguza mavuno kwa asilima 100%






2.      Ugonjwa wa Madoa ya Majani (leaf spots)
Ugonjwa huu ni wa aia mbili yaani madoa changa ( Early Spot) na madoa pevu (Late Spot). Hupunguza mavuno kwa asilima 30%







3.      Ugonjwa wa Kutu ya Majani (Rust)
Husababishwa na vimelea vyaPuccinia arachidis. Jani huwa na vipele vya rangi ya kahawia has chini ya Jani.










4.      Sumu Kuvu ya karanga (aflatoxin)
Katika hali ya unyevu mwingi vimelea viitwavyo Aspegilus flavus huota ndani ya maganda na kushambulia mbegu za karanga. Vimelea hivyo hutoa kemikali ambayo ni sumu.









Kudhibiti Magonjwa
Magonjwa ya karanga yanaweza kudhibitiwa kwa kutumia mbegu bora zenye ukinzani, kupanda mapema, kupanda katika nafasi zilizopendekezwa, kukausha mavuno na kuhifadhi mahali pasipo na unyevu.







Wadudu waharibifu
Vidukari, Inzi, wa karanga, Mchwa, Panya na Ndege. Dhibiti kwa kupanda mapema, kupanda kwa nafasi, kutumia kilimo mseto na kupuliza viuatilifu.

UVUNAJI NA UHIFADHI
Vuna baada ya kukomaa kwa jembe la mkono au kung’oa. Kausha vizuri kwenye jua kwa muda wa wiki 2 – 3 hadi kufikia unyevu wa chini ya 13%. Karanga zilizokauka vizuri hutoa mlio ukitikisa ganda lake. Hifadhi kwenye ghala kavu zikiwa kwenye magunia yanayopitisha hewa na zikiwa na maganda yake. Ubora wa karanga kuota huanza kupotea mara baada ya kubanguliwa.