Karanga ni zao muhimu la mafuta ambalo hutumika kama chakula cha binadamu. Mashudu na majani yake hutumika kulisha mifugo. Pia hurutubisha udongo. Tanzania ni nchi ya pili kwa uzalishaji wa karanga Afrika baada ya nchi ya Nigeria. Karanga hustawi zaidi Mikoa ya Mtwara, Dodoma, Shinyanga na Tabora.
Mazingira ya ustawishaji
Karanga hustawi vizuri katika maeneo yenye mwinuko chini ya Mita 1500 kutoka usawa wa Bahari. Huhitaji mvua ya wastani wa milimita 500 – 1200 kwa mwaka. Pia hustawi vizuri kwenye udongo wa kichanga wenye rutuba.
Utayarishaji wa Shamba
Tifua vizuri shamba ili kuwezesha udongo kupenyesha maji na mizizi kirahisi. Karanga hupandwa kwenye matuta au sesa.
Kuchagua mbegu za kupanda
Hakikisha unapata mbegu bora za karanga zilizothibitishwa kitaalamu na kuainishwa na Taasisi za Utafiti wa Kilimo.
AINA ZA KARANGA
Kuna aina tisa za mbegu za karanga ambazo zimefanyiwa utafiti na kuidhinishwa zitumike kwa wakulima nazo ni:
Pendo 1998
Hukomaa kwa wastani wa siku 90 – 100 na hutoa mavuno ya wastani wa tani 1.5 kwa hekta. Ina mafuta ya wastani wa asilimia 48.
Naliendele 2009
Hukomaa kwa siku 90 – 100 na hutoa mavuno ya wastani wa tani 1 kwa hekta. Huvumilia ukame na ugonjwa wa ukoma.
Mangaka 2009
Hukomaa kwa siku 90 – 100. Huzaa mbegu 2 – 3 kwenye ganda moja. Hutoa mavuno wastani wa tani 1.5 kwa hekta. Ina mafuta wastani wa asilimia 48.
Mnanje 2009.
Hukomaa kwa siku 110 – 120. Hutoa mavuno ya wastani wa tani 1.5 kwa hekta. Ina mafuta wastani wa asilimia 51
Masasi 2009
Hukomaa kwa siku 110 – 120. Hutoa mavuno ya wastani wa tani 1 kwa hekta. Huvumilia ugonjwa wa ukoma na ina mafuta wastani wa asilimia 50.
Nachingwea 2009
Hukomaa kwa siku 110 – 120. Hutoa mavuno wastani wa tani 1 kwa hekta.
Nachi 2015
Hukomaa kwa siku 110. Hutoa mavuno wastani wa tani 1.1 – 2 kwa hekta. Huvumilia ugonjwa ya Ukoma
Kuchele 2013
Hukomaa kwa siku 102 – 110. Hutoa mavuno wastani wa tani 1.2 – 2 kwa hekta. Huvumilia magonjwa ya Ukoma, kutu na madoa ya majani.
Narinut 2015
Hukomaa kwa siku 106 – 110. Hutoa mavuno wastani wa tani 1.2 – 2 kwa hekta. Huvumilia magonjwa ya Ukoma, kutu na madoa ya majani.
Upandaji
Mbegu zipandwe mapema wakati wa mvua za kwanza. Karanga zipandwe kwa nafasi ya entimita 10 kati ya mmea na sentimita 50 kati ya mstari. Kilo 80 hadi 100 za mbegu zitahitajika kupanda hekta moja kwenye shimo la kina kati ya sentimita 2.5 hadi 5.
Palizi
Palizi ya kwanza ifanyike majuma mawili baada ya karanga kuota. Palizi ifanyike mara mbili hadi tatu kuzuia magugu.
KUDHIBITI WADUDU NA MAGONJWA
Magonjwa
1. Ugonjwa wa ukoma ( Rossette Virus diseases)
Huenezwa na wadudu waitwao Vidukari (aphids). Mimea inayoshambuliwa hudumaa, majani kukunjamana na kuwa na rangi ya manjano. Pia hupunguza mavuno kwa asilima 100%
2. Ugonjwa wa Madoa ya Majani (leaf spots)
Ugonjwa huu ni wa aia mbili yaani madoa changa ( Early Spot) na madoa pevu (Late Spot). Hupunguza mavuno kwa asilima 30%
3. Ugonjwa wa Kutu ya Majani (Rust)
Husababishwa na vimelea vyaPuccinia arachidis. Jani huwa na vipele vya rangi ya kahawia has chini ya Jani.
4. Sumu Kuvu ya karanga (aflatoxin)
Katika hali ya unyevu mwingi vimelea viitwavyo Aspegilus flavus huota ndani ya maganda na kushambulia mbegu za karanga. Vimelea hivyo hutoa kemikali ambayo ni sumu.
Kudhibiti Magonjwa
Magonjwa ya karanga yanaweza kudhibitiwa kwa kutumia mbegu bora zenye ukinzani, kupanda mapema, kupanda katika nafasi zilizopendekezwa, kukausha mavuno na kuhifadhi mahali pasipo na unyevu.
Wadudu waharibifu
Vidukari, Inzi, wa karanga, Mchwa, Panya na Ndege. Dhibiti kwa kupanda mapema, kupanda kwa nafasi, kutumia kilimo mseto na kupuliza viuatilifu.
UVUNAJI NA UHIFADHI
Vuna baada ya kukomaa kwa jembe la mkono au kung’oa. Kausha vizuri kwenye jua kwa muda wa wiki 2 – 3 hadi kufikia unyevu wa chini ya 13%. Karanga zilizokauka vizuri hutoa mlio ukitikisa ganda lake. Hifadhi kwenye ghala kavu zikiwa kwenye magunia yanayopitisha hewa na zikiwa na maganda yake. Ubora wa karanga kuota huanza kupotea mara baada ya kubanguliwa.
No comments:
Post a Comment